Search

Sunday, January 14, 2007

Uwajibikaji uko wapi kwa viongozi wetu?
Nini maana ya kuwa kiongozi wa umma? Je wengi wa viongozi wetu wanaelewa dhana hii nzima ya kuutumikia umma au jamii? Je walioko madarakani na wanaoongozwa wanaonyesha na kufahamu wajibu wao kwa jamii na kuwa viongozi bora wa kuigwa na kizazi chetu cha baadae? Haya ni baadhi ya maswali ambayo nitajaribu kuyaongelea katika makala yangu hii.

Kwa Tanzania ni dhahiri kuwa moja kwa moja wengi wa viongozi walioko madarakani katika sehemu mbali mbali mbali serikalini na katika taasisi mbalimbali wameshindwa kuwa ni mfano bora wa mtu mwadilifu anayeongoza jamii anavyopaswa kuwa. Wamekuwa ving’ang’anizi wa madaraka na kusahau kuwa umma unawaangalia na katika umma huu kuna watu wa silka, umri na uwezo mbalimbali wa kuchambua mambo katika jamii.


Ni kwanini viongozi wetu hawataki kuwa mfano bora kwa jamii inayowaangalia. Matatizo mbalimbali yanatotukabili, likiwemo hili la umeme ambalo ni moja ya nguzo kuu katika maendeleo ya taifa lolote ni sababu ya kutokuwa na uadilifu kwao. Hao tunaowaita kuwa wameendelea kitu kikubwa cha maendeleo yao ni kuwa na umeme wa uhakika, kwani bila ya umeme hakuna uzalishaji na matokeo yake ni kutokuwa na ziada ya kuuza nje na kujiongozea mapato.

Kwanini hatukubali kuwa tumeshindwa katika kuongoza na kuwaachia wengine waendelee kufanyia kazi pale tuliposhindwa? Hili ni tatizo na nafikiri umefika wakati sasa wa wale walioko madarakani kutambua hilo na kuirudisha hiyo tabia ili wawe ni miongoni mwa viongozi wa kuigwa na kukumbukwa hapo baadae kutokana na uongozi wao.

Inasikitisha na inatia aibu kwa jinsi hali ilivyo sasa. Kiongozi anapokuwa madarakani na kusemwa na ushahidi kutolewa kwa kuvuruga katika utendaji wa kila siku lakini wanakuwa jeuri na kujifanya hana habari hao wasemaji wote ni wendawazimu tu kwako, hawawezi kukuharibia wewe utaratibu wako wa “kula nchi”. Ndio tunasema kula nchi kwani kama wangekuwa wanajali maendeleo ya hao waliowaweka madarakani basi wangeogopa na kuomba kuwaachia wengine kufanya hizo kazi wazifanyazo.

Katika historia ya nchi hii ni viongozi wachache sana waliofikia mahali wakawajibika kutokana na nafasi zao mbali ya kuwa sio wao waliofanya makosa sembuse hawa ambao hivi sasa tunawaona moja kwa moja kuwa wao ndio wahusika wakuu lakini hawana hata hofu ya kukubali kuwa cheo ni dhamana na sio kama ni mali yao ambayo tumewapa wakae nayo daima.

Hivi karibuni tumesikia huko Japan kiongozi katika Serikali ya Waziri Mkuu Kinzo Abe amewajibika baada ya magazeti kutoa taarifa kuwa anatumia pesa za kodi ya wananchi kula maisha na kimada wake wakati ana mke amemuacha katika mji mwingine. Leo Tanzania hii wako wanaoshutumiwa kwa zaidi ya hayo lakini mnaosema mnaonekana ni wababaishaji tu, tunakwenda wapi viongozi?

Ni aibu kwa kiongozi kushutumiwa kuwa yuko nje ya maadili ya Taifa nab ado kung’ang’ania kukaa madarakani. Aibu hii inazidi pale ambapo wananchi nao wanaposhindwa kujua wafanye nini kutokana na shutuma kwa kiongozi husika. Inashangaza zaidi wakati tuna tume ya maadili ya viongozi jee wameshindwa kufanya kazi? Au wajibu wao uko katika kutangaza mali tu viongozi wanapoingia madarakani? Nafikiri ni wakati muafaka sasa tukajaribu kujiangalia na kufanya marekebisho ili kuwe na mfano wa kuigwa kwa wajao hapo baadae.

Tanzania kama tunataka maendeleo ya kweli basi hatuna budi kupiga kelele na kushutumu huu utaratibu ulioko asa wa viongozi kutotaka kuwajibika kutokana na dhamana tulizowapa! Inasikitisha kuwa mara baada ya kupewa dhamana mhusika anabinafsisha na kufanya hiyo dhamana ni mali yake binafsi haipendezi na sio katika kuwajibika kwa wale waliokupa dhamana ya kuwaongoza.

Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kusema kuwa hawataki kuwajibika kama ambavyo tumezoea kuwasikia wakisema mara kwa mara pale ambapo shutuma dhidi yao zinapotolewa. Sina uhakika kama wanaelewa maana ya uongozi ni nini. Kwa tafsiri nyingine ambayo mimi huwa naiona ni kwamba kuna kulindana kutokana na makosa wanayofanya viongozi kati yao. Maana inakuwaje wakati ushahidi upo bado kiongozi anang’angania madaraka!

Hii inaonesha dhahiri kuwa kama sio wote, walioko madarakani wakiwemo wabunge kuwa wote ni wachafu na sio waadilifu katika dhamana tulizowapa. Kwani kama hakuna kulindana kwanini mtu asiambiwe dhahiri shahiri kwamba “ee bwana we umekosea ondoka” kwani akiachia madaraka ndio utakuwa mwisho wa maisha yake? Hii inaonesha ni jinsi gani ubinafsi ulivyotutawala.

Inajulikana wazi kuwa tabaka la viongozi limekusanya watu wachache na kwa vyovyote vile wanajuana katika maisha yao ya kila siku. Kwani ni nadra sana kwa mtu wa chini kushirikiana na mtu mwenye kipato cha juu. Hivyo walioko madarakani ni kawaida kushirikiana na kuwa pamoja miongoni mwao na ndio maana nikasema kuwa wanalindana na hivyo wanashindwa kusemana na kukemeana kwani lao ni moja. Hii ni aibu kwa Taifa.

Katika kuchukua dhamana za watu kiongozi anatakiwa awe na moyo wa kuwatumikia hao waliomchagua na sio kujali maisha yake na familia yake tu kama ambavyo hali ilivyo sasa. Sihitaji kutoa mifano hapa kwani kwa mada hii hili si jambo geni ndani ya jamii yetu ya Tanzania. Ile dhana ya kuitumikia jamii imeshakufa na kupitwa na wakati. Hapa nchini kwetu kila aingiaye madarakani anafikiria kujinufaisha binafsi na waliomzunguka.

Mifano imejaa tele kwani hivi sasa uongozi umekuwa ni mradi wa kutajirika na wala hakuna anaeuliza mara baada ya kiongozi kuwa madarakani maisha yake kwa ujumla yanabadilika na kuwa ni mtu wa juu kupita wote ndani ya jamii husika. Inashangaza lakini hii ndio hali halisi kwa Tanzania yetu ya leo. Hatukatai mabadiliko lakini hali iliyoko sasa inakatisha tamaa kwa wanaojua maana ya kuwa kiongozi wa umma.

Kauli ya Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni wakati akisherehekea mwaka mmoja tokea serikali yake kuingia madarakani ya kukataa kupewa sifa za kinafiki na za kujipendekeza naona kama vile inaweza kuanza kufungua akili katika vichwa vya hao walioko madarakani na kuwa na mustakbali mpya kuwa sasa wanapaswa kuwa makini zaidi na aliyeshindwa ni bora tu aondoke madarakani kwa heshima kuliko kupata aibu.

Rais Kikwete amekataa sifa za kinafiki na za kujipendekeza ambazo wengi wa viongozi wanapenda kuzipata na kuzitoa kwa wakubwa zao wakati wajua dhahiri kuwa wanachokisema hakiko hivyo. Hii yote ni mjumuisho wa matatizo ya uwajibikaji kwa viongozi na wananchi ndani ya Tanzania yetu. Ni makosa makubwa na hatuwezi kupata maendeleo hata siku moja kama hatujabadilika na kuacha tabia hii mbovu.

Ni utamaduni wetu Watanzania sio siri wa kusifia makosa na pale mmoja miongoni mwetu anapotaka kusema ukweli huambiwa ni msaliti wakati anachotaka kukisema au alichosema ni cha haki na ukweli kabisa. Tubadilike viongozi na wananchi kwa ujumla huu sio wakati tena wa kuwaachia watu wachache wakitupeleka peleka katika lindi la umasikini na matatizo kutokana na ubinafsi na ulafi wao tu. Kama tunaona makosa na tunamjua aliyeyatenda hatuna budi kusema na sio kufichua majambazi tu. Kiongozi anayevuruga wananchi hana tofauti na jambazi yoyote yule.

Huu sio uchochezi bali ni haki ya kila mmoja kutokana na haki za msingi kabisa za binaadamu katika uhuru wa kujieleza kama zilivyopitisha katika Umoja wa Mataifa na pia kama zilivyoainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama kinachosemwa ni cha ukweli na kina ushahidi basi ni haki yako kukisema na hiyo ni katika kuleta maendeleo na kulinda maslahi ya Taifa kwa ujumla.

Uzalendo wetu kama Watanzania tunaoipenda nchi hii ni kubainisha yale machafu ya viongozi na sio kuwa wanafiki. Ilishasemwa zamani kuwa “Ukweli ni mchungu, hatuna budi kuusema japo unauma” tuseme ukweli bila ya hivyo matatizo yetu hayawezi kwisha kwa kutegemea wanafiki na walioingia madarakani kwa maslahi binafsi. Ripoti tofauti za wanaotufadhili zimeshalisema hili kuwa moja ya matatizo katika nchi zinazoendelea, viongozi kutokuwa waaminifu kutokana na utendaji wao.

Nchi yenye demokrasia ya kweli wananchi wake wana uhuru wa kuzungumza na hapo ndio maendeleo ya nchi yanapopatikana. Tufike mahali hasa katika kipindi hiki tulichonacho sasa tuwe na utamaduni mpya katika kuonyesha uwajibikaji wetu kwa jamii iliyotukabidhi madaraka na pia kwa maendeleo ya Taifa letu.

Kiongozi unapovuruga leo kwa ajili ya maslahi ya sasa hivi awe na uhakika kuwa atakayekuja athirika hapo baadae ni jamaa anayemhusu mwenyewe kama sio wajukuu zake. Hata siku moja hatotokea mtu toka nje ya nchii hii kuja kutuletea maendeleo ila ni sisi wenyewe tunapaswa kujiletea hayo maendeleo, nayo ni kuwajibika kutokana na dhamana tulizopewa na sio kuipelekea kuzimu nchi yetu kama hali ilivyo sasa.

Tabia mbovu iliyoko sasa hivi ya kudharau watu wa kipato cha chini au wasio na madaraka na kuwaona kuwa hawana nafasi katika maendeleo ya nchi hii wakati wanalipa kodi haina budi kuachwa. Hakuna ambaye hana haki, ili mradi ni mwananchi na analipa kodi kwa ajili ya kulipia mshahara wa wewe uliyeko madarakani basi huna budi kumstahi na kupokea na kukifanyia kazi kile anachokisema. Simaanishi kuwa kila kinachosemwa kuwa kina maana vingine havina lakini kama kiongozi hupaswi kudharau kama ambavyo tunaona sasa katika Tanzania hii.

Na labda hapa ndipo ambapo wengi wa waliopewa dhamana wamepasahau kabisaa. Kama mwananchi analipa kodi ni moja kwa moja anachangia mshahara na maendeleo ya Taifa hili hivyo asikilizwe na aheshimiwe badala ya kufanyiwa dharau kama ambavyo ilivyo sasa. Kwenye hili kuna mifano mingi sana mojawapo iweje leo watu waandamane na kutaka kumuona rais wakati waliokabidhiwa dhamana za kuwahudumia wapo? Watu wamekuwa na imani na Rais zaidi kuliko ya hao waliopewa dhamana kumsaidia katika kuongoza! Inatisha!.

Kiongozi wa umma anawajibika kwa umma uliomuweka madarakani na sio kusema kuwa hana nafasi na yuko na shughuli nyingi za kiofisi, mimi nafikiri nafasi ya kwanza ni kupewa huyu anaechanga ili wewe uliyeko madarakani upate mshahara, ingawa kuna watakaobeza kauli hii na kusema labda ni fedha ndogo sana mwananchi huyu anachangia, hata kama hachangii pia anapaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa, kwa vile mmekubali dhamana ya kuwatumikia wananchi wote.
Uamuzi wa hivi karibuni wa wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuamua kuendesha mafunzo kwa jamii ya Wazanzibari inatokana na kushindwa kwa viongozi kuwajibika kutokana na nafasi tulizowapa kutuongoza. Kama wangetuongoza vizuri na kuwajibika pale waliposhindwa naamini tusingefikia leo hii tunafunguliwa Chuo na kupewa mafunzo maalum kwa ajili ya kufunzwa kuwajibika na kutunza uzalendo wetu.

Hii inaonyesha jinsi ya ukubwa wa tatizo la viongozi kutowajibika kutokana na nafasi zao ndani ya nchi hii lilivyo. Hata ukiangalia sheria nyingi zilizoko zinaonyesha upande mmoja katika jamii ambavyo unavyopaswa kuwajibika na kutekeleza majukumu yake lakini upande wa pili wa walioko madarakani sheria nyingi haziko wazi na zimefichwa kwa jamii na matokeo yake mmojawapo anapotoa changamoto anaonekana ni mchochezi, asiyefuata sheria na majina mengi tu kupewa na kuwajibishwa kutokana na sheria zilizopo za upande mmoja.

Ni wakati umefika sasa wa kuanza upya baada ya miaka 45 tokea nchi hii kuanza kujitawala tukaanza kujenga Taifa la viongozi na wananchi wanaowajibika kutokana na nafasi zao kwa maendeleo ya Taifa hili. Rais Kiwete ameonesha njia tunapaswa sasa kuipalilia njia hii ili tuweze kufika kule ambako wenzetu nao wamefika. Inajulikana dhahiri changamoto ni nyingi basi tupambane na zile zilizoko nje na sio sasa kama hali ilivyo ya kwamba tunapambana na za ndani na nje kwa wakati mmoja.

Unapowajibika kutokana na nafasi ya uongozi inaonesha ni jinsi gani ulivyokuwa kimaadili na pia inaonyesha kuwa hukuzaliwa kuwa kiongozi, katika kuongoza unapaswa kushirikiana na wengine hivyo unapoachia ngazi na kumpisha mwengine hiyo yote ni katika kuliendeleza gurudumu la maendeleo ya nchi na taasisi mbalimbali zilizoko ndani ya jamii yetu.

Mara zote wanaoachia ngazi mapema kutokana na kuonyesha kukubali kwao kuwa wamefanya makosa wanapata heshima kubwa ndani ya jamii na sio wale ambao wanang’ang’ania madaraka ambapo wengi matokeo yake ni kupata aibu na kashfa ndani ya jamii husika na hata pale wanapoondoka madarakani wanakuwa na shutuma hadi umauti unapowafika. Sasa ni lipi bora kama wewe ni kiongozi, kuwa na heshima na watu kuja kutaka ushauri kwako wakati ukiwa huna madaraka au kubakia na shutuma na kukulaani hadi unaingia kaburini ukiwa na madaraka yako?

No comments:

At class - MUM

At class - MUM
Mazoezi ya uhariri wa picha kwa kutumia kompyuta Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro - MUM

Mjadala studio

Mjadala studio
Wanafunzi wa shahada ya kwanza mawasiliano kwa umma mazoezini studio za Muslim University of Morogoro