Search

Sunday, January 14, 2007

Tangazo la condom na utamaduni wa Mtanzania
Uamuzi wa kukataa jambo ni wa mtu binafsi ingawa mazingira nayo yanachangia kwa kiasi kikubwa juu ya uamuzi huo. Kweli tuko katika dunia huru – dunia kijiji kimoja, lakini mazingira ya nchi moja na nyingine ni tofauti kutokana na utamaduni na silka za watu wake. Jambo lifanywalo na nchi moja isiwe ni sababu ya kufanywa au kufuatwa na nchi nyingine kwa sababu ya utandawazi, naamini uhuru wa kuamua kufuata au kutofuata bado tunao hatujanyang’anywa uhuru huo.

Nasema haya kwa sababu sasa hivi wananchi tunanyang’anywa uhuru wetu kwa nguvu zote kutokana na nguvu walizonazo wamiliki wa vyombo vya habari. Kwanini? Nitazungumzia tangazo la kondomu aina ya Salama (Studded) “zenye vipele”. Hilo tangazo sio siri naamini wengi wetu linatunyima uhuru wetu ndani ya nyumba zetu tukiwa na familia zetu.


Mbali ya tangazo hili kutunyanyasa kijinsia wanaume, kilichomo ndani ya tangazo hili ni udhalilishaji wa moja kwa moja kwetu. Hebu niulize hivi kweli sehemu za siri za mwanaume zinaweza kuwa mfano na chakula tunachokula? Inakuwaje leo tuchukue chakula na kukifananisha na sehemu hizo? Najua wako watakaosema ndio kwani uongo hazifanani, sawa zinafanana lakini sio utamaduni wetu kulinganisha chakula na sehemu hizo halafu tukaweka hadharani tunaangalia na watoto wetu!

Ndio maana nikasema awali kuwa huu utandawazi na kuwa kijiji kimoja sio kwa kila kitu, vyombo vya habari vinapaswa kulizingatia hilo, kila sehemu kuna tabia na mambo yao sasa sio lazima ujumbe ufikishwe kwa njia kama iliyotumika kwengineko, mnaweza kuleta vurugu ndani ya jamii kama itokeavyo sasa kutokana na tangazo hili, au tunasubiri hadi watu waandamane ndio tushituke?

Hili tangazo halifai kwa jinsi lilivyotengenezwa, kwetu naamini wengi wetu ni matusi ya moja kwa moja na udhalilishaji. Baya zaidi ukiangalia matiririko mzima wa tangazo hilo kwani sio wanaume pekee waliodhalilishwa hadi mama zetu tena wazee! Inawezekana kuwa linakubalika kwengineko wenye utamaduni huo lakini kwetu halikubaliki kwa mtazamo wangu, walio na jukumu na tangazo hilo walibadilishe.

Hatukatai kuwa vita dhidi ya ukimwi ni ya kila mmoja katika jamii lakini mbinu haziwezi kuwa sawa katika kupambana na janga hili kwa kuzingatia silka na tamaduni zetu kutofautiana na ndio maana watu wanakutana kila siku katika semina na makongamano ili kupata mbinu sahihi za kupambana na janga hili na sio kutumia mbinu za sehemu moja na kusema kuwa tutapata mafanikio.

Kila kitu kina hadhi na heshima yake, chakula siku zote ni chakula hakiwezi kufika mahali kikafananishwa na kitu kingine, kama wanafanya ni wao lakini sio sisi. Na hii ndio maana kuna baadhi ya mambo kwa wenzetu huko walikoendelea kwao ni sawa lakini sio hapa kwetu, mfano ni hizo ndoa za jinsia moja tunajua kuwa wapo watu wa aina hiyo ndani ya nchi yetu lakini katika utamaduni wetu haziruhusiwi na ndio maana hazijapewa nafasi sasa iweje tuonyeshe matusi hadharani.

Tusifike mahali tukawa kama tusiofikiri tulinde utamaduni wetu. Suala la kufikiria maslahi binafsi bila ya kuangalia athari zake kwa jamii linapaswa kuzingatiwa. Tunaelewa kuwa wamiliki wanafanya biashara lakini biashara hiyo ni kwa maslahi ya nani? Suala la kuweka ubinafsi hapa unaweza kutumbukia nyongo na kusababisha adha kwa wahusika, chambilecho mtu akaona anachukiwa halafu akasema nachukiwa tu sijaona kosa lolote nililofanya.

Kama tunafika mahali tunakamata vitabu na machapisho ya ngono, inashangaza tunaruhusu tangazo lenye matusi moja kwa moja hadharani, inashangaza kidogo, au kwa vile anaetangaza ana pesa hawezi kudhibitiwa au ni ubinafsi tu ndio tumeuweka mbele bila ya kujali maslahi ya jamii husika? haya ni baadhi ya maswali ambayo huwa yananipita kila mara nionapo tangazo hili.

Tuheshimu uhuru na haki za binaadamu, hili huwa napenda kulirudia mara kwa mara. Mara zote uhuru wa mtu mmoja au kundi fulani usiwe madhila na mateso kwa wengine. Sawa tunasema tutazoea lakini jee ndio tunatengeneza jamii au ndio tunaiharibu, hebu na tunagalie hizo jamii ambazo tunaziita wameendelea matatizo waliyonayo katika jamii zao kutokana na uhuru huo ambao nasi tunataka kuzipa jamii/familia zetu.

Tuende mbele na kurudi nyuma tusiige tu kila kitu kwa maslahi ya wachache, tutafika mahali kama hatujafika bado tushindwe kabisa kuwa na uwezo wa kuyakabili matatizo ambayo yatajitokeza kutokana na uhuru huu wa kujieleza tunaoipa jamii yetu kupitia vyombo vyetu vya habari. Tuwe waangalifu kwenye hili wao huko walianza hivi hivi na matokeo yake tunayaona.

Ni changamoto kwa serikali na jamii kwa ujumla kuipa na kuiwezesha fani ya utungaji na utengenezaji filamu na matangazo nchini uwezo kwa maana ya mazingira na uwezo wa kuzalisha kile ambacho kitakuwa na maslahi kwa jamii yetu na sio kupokea tu kila kinachozalishwa tuko nje ya nchi kama hali ilivyo sasa.

Serikali haina budi kuwekeza kwa makusudi kabisa katika fani hii na tusirudie kosa ambalo limefanyika la kufuta na kuiua fani hii kama vile walivyoua Kampuni ya Filamu Tanzania, hii kampuni inapaswa kufufuliwa upya ili mawazo na vitendo vinavyoonyeshwa katika filamu basi vilingane na tamaduni na silka zetu na sio uchafu ambao umezagaa hivi sasa kila kona ya miji yetu.

Matokeo ya kuua hii fani ndio haya tunaletewa filamu na matangazo ya ajabu mbele ya jamii na familia zetu, mara lionyweshapo basi mzazi huna budi kutafuta udhuru wa muda ili uepukane na maumivu ya aibu ambayo utayapata kwa sekunde /dakika chache tangazo au kipindi kikiwa hewani.

Lazima tufike mahali tuone kuwa kinachozalishwa kinakidhi maslahi ya pande zote mbili yaani wazalishaji na wanaopelekewa kutumia hiyo bidhaa. Kwanini tuna mashirika ya kuthibiti viwango kwenye vyakula na ubora wa vifaa mbalimbali kama Shirika la Viwango Tanzania – TBS, na kwanini tusiwe na taasisi kama hiyo kwenye kile kinacholetwa kwa jamii toka kwa mtu yeyote na hii yote ni katika muktadha ule ule tu wa kulinda na kuheshimu haki ya kila mmoja bila ya kusahau utamaduni na silka za jamii yetu.

Tumeona na tunashuhudia faida za sekta hii ndani ya jamii yetu hivi sasa baada ya kupewa uhuru imewapatia kazi vijana wengi hivi sasa, filamu na muziki pamoja na matangazo mengi yanazalishwa lakini kutokana na ubovu, ughali na mazingira magumu katika uzalishaji wa vitu hivyo tumeshindwa kupata bidhaa bora ambazo zinaweza kushindana katika soko la kimataifa.

Kupitia kwa wawekezaji na serikali yenyewe inawezekana kabisa sekta hii ikaboreshwa na kuwekewa mazingira mazuri na tukapata bidhaa ambazo zinalingana na utamaduni wetu nasi tukawa na cha kuuza na kuringia katika masoko ya kimataifa badala ya sisi kuwa soko la bidhaa hizo ambazo hazina heshima wala maadili na tamaduni zetu. Utamaduni wa Tanzania ni tajiri sana kutokana na makabila zaidi ya mia moja yaliyoko katika nchi hii.

Mbinu za kuwasilisha ujumbe na ukakidhi maswali na matatizo yaliyopo nina hakika zipo ila hazijapewa nafasi yake na badala yake tunathamini na kusisitiza bidhaa toka nje kwa kuona ndio bora na zinazokubalika, kitu ambacho sio kweli nyingine zinalazimishwa tu tuzikubali lakini zinatuathiri na hatuna budi kuanza kusema sasa.

Kwanini tunakubali kuwa watumwa ndani ya nchi yetu, nasema hivyo kwa sababu mawazo yaliyopo ni kwamba hatuwezi kuzalisha bidhaa kama muziki, filamu au tangazo litakalowakilisha utamaduni na maadili yetu. Ili kukidhi mahitaji ya soko lazima tuingize matendo ya hao wanaoitwa wameendelea! Naamini tuna mengi tu ambayo na hao walioko nje nao pia wanapaswa kujifunza kutoka kwetu kwanini hatutumii nafasi hii ya utandawazi!?


Mbona nchi za wenzetu wameweza kwanini sisi tushindwe? China kwa mfano wamewawekea masharti makampuni makubwa ya Marekani kama Google kwamba yasiruhusu uchafu wa picha za ngono katika mitandao yao huko China na wamekubali hilo kwanini sisi tushindwe! Inashangaza na inasikitisha jambo hili au kwa vile hatuna nguvu za kiuchumi? basi hiyo iwe changamoto kwetu ili tuondokane na adha na madhila tunayoyapata.

Uwezekano wa sisi kuzalisha kilicho bora upo cha muhimu ni kuweka mikakati inayotekelezeka kwa wote walioko katika fani hii ya habari na mawasiliano. Imefika wakati wa kuziona changamoto hizi na kuzifanyia kazi. Dunia hii ya utandawazi ina changamoto nyingi sana ambazo hatuna budi kukabiliana nazo kwa mbinu zote zile na sio kukubali kuwa soko la kila kinachotoka kwa hao walioendelea wanatupeleka pabaya na tusipoangalia tutajikuta mahali ambapo hatuwezi tena kutoka.

No comments:

At class - MUM

At class - MUM
Mazoezi ya uhariri wa picha kwa kutumia kompyuta Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro - MUM

Mjadala studio

Mjadala studio
Wanafunzi wa shahada ya kwanza mawasiliano kwa umma mazoezini studio za Muslim University of Morogoro