Nini maana ya kuwa mhitimu katika fani au sekta husika? Je Watanzania wasomi tunaelewa maana halisi ya kujishughulisha na fani/utaalamu fulani au kusomea fani hizo kama ijulikanavyo na wengi wa wanafunzi katika Vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ya juu hapa nchini? Ionekanavyo ni bado hatujaweza kuzitumia fani/taaluma hizo kwa maendeleo ya nchi yetu, Je tatizo liko wapi na ni kwanini basi kuwepo na hali hiyo? Fuatilia makala hii ili tusaidiane mawazo katika kueleweshana na kujaribu kupata ufumbuzi wa tatizo hili ndani ya jamii ya watanzania.
Ni wangapi walioko katika fani mbalimbali hapa nchini wanaweza kujivuna kuwa wamechangia kwa kiwango cha kupigiwa mfano au hata kiwango cha chini kabisa katika fani zao? Kama ni kuwataja basi itakuwa ni wachache sana ikilinganishwa na idadi ya waliosomea fani/taaluma hizo husika. (Najua sio wengi kama ipasavyo kuwa). Ni katika siasa tu ambako kwa matazamo wangu kuna mengi lakini mimi sitazungumzia huko. Sina maana kuwa sithamini mchango wa wanasiasa, la hasha ila katika makala hii sikusudii kuangalia masuala ya wanasiasa.