Search

Sunday, January 14, 2007

Dhana ya Ujasiriamali na utendaji wa viongozi Tanzania
Nitazungumzia dhana ya ujasiriamali na utendaji wa viongozi wetu na mazingira yao katika taasisi na sekta mbalimbali kwa ujumla hapa Tanzania. Kwani mengi ya matatizo ambayo tunakumbana nayo sasa hivi katika maisha, uendeshaji na utekelezaji wa kazi kila siku kwa matazamo wangu ni kutokana na viongozi hao kukosa au kutoelewa maana halisi ya ujasiriamali.

Hivi sasa wengi tumeichukulia na kuihusisha dhana hii na upande wa biashara tu, jambo ambalo ni kosa kubwa tunalolifanya na inawezekana ikawa ndio sababu ya kuwa na matatizo lukuki ndani ya jamii bila ya kuwa na suluhisho nayo kwa sababu viongozi tulionao hawana au hawaelewi dhana nzima ya ujasiriamali.


Ni hivi karibuni tu nchi hii imeanza kuitumia dhana hii kwa ajili ya kujiletea maendeleo, lakini kubwa ni kwamba wanaofundishwa ni wale walioko katika elimu ya juu na kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa, lakini sijasikia kama viongozi na walioko madarakani wanapewa elimu hii ya ujasiriamali na kama wamepata basi hawajaitumia ipasavyo katika kutuletea madabiliko na hatimae maendeleo katika nchi hii.

Ili ujasiriamali uweze kutoa matokeo yanayotarajiwa au mjasiriamali anatakiwa kuwa ni mwepesi wa kufikiri na kuamua, mwenye uwezo wa kubaini nafasi za maendeleo katika fani aliyoko, kutumia nafasi na uwezo wake katika kuleta maendeleo kwa haraka, kuwa na uwezo wa kuwa na mtandao na mawasiliano ya karibu na wote wanaoshiriki na kuendeleza fani au sekta husika aliyoko, mwenye kuwajibika, mwenye kukubali na kukabiliana na changamoto zinazomkabili kwa njia zote na mengine mengi ambayo yanayomfanya mtu awajibike na kuendelea kwa haraka katika sekta au fani aliyoko.

Sasa ukiangalia kwa makini wengi wa viongozi wetu katika sekta mbalimbali ndani ya jamii hawana au hawataki kuwa na sifa zilizotajwa hapo juu. Na moja kubwa ni kwamba huwa hawakubali changamoto wanazokumbana nazo katika utendaji wao wa kila siku na matokeo yake ni migogoro na mizozo inayopatikana katika maeneo yao na moja ya sababu kubwa ikiwa ni kutokuwepo na mawasiliano na mitandao baina ya pande husika.

Siku zote katika utawala na utendaji wa kazi kama kuna mawasiliano na mtandao baina ya pande husika hutoweza kusikia mizozo na migogoro. Hivi sasa katika nchi hii ukienda vyuoni, viwandani, ofisini, shuleni, katika makampuni, ili mradi kila sehemu watu wanatumia muda mwingi wa kazi kutatua mizozo na migogoro mbalimbali inayowakabili jambo ambalo kama wahusika wangekuwa na dhana ya ujasiriamali ndani ya vichwa vyao jambo ambalo lingeweza kuepukw na tungekuwa mbali hivi sasa kutokana na muda huo kutumiwa kwa kujiletea maendeleo.

Jambo ambalo naliona mimi kwa mtazamo wangu ni kuwa tutachelewa sana nchi hii kuendelea kama hatujabadilika na kuwa na fikra na mawazo kama ya wenzetu katika nchi zilizoendelea. Viongozi wanapaswa kuwa wepesi wa kukubali changamoto na kukabiliana nazo na sio kuzikimbia kwa kutafuta visingizio vya aina mbalimbali.

Naamini waliokaa na kufikiria kuingiza somo la ujasiriamali ndani ya mitaala ya vyuo vikuu wameona mbali na hawana budi kupongezwa kwa hilo kwani tunategemea viongozi wajao watakuwa wepesi katika kutatua na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta mbalimbali nchini ili kuleta maendeleo kwa haraka.

Tukichukulia mfano wa hali ilivyo hivi sasa wengi wa wahitimu wa elimu ya juu hapa nchini kupata kwao ajira kunakuwa na mtihani kidogo tofauti na wale waliosomea nje ya nchi. Kwani waliosoma nje wanaonekana wako makini, wajanja, wabunifu, wepesi wa kuchukua hatua, wanaona mbali, wanatumia kwa ukamilifu nafasi zilizopo, na kadhalika na hizo zote ni miongoni mwa sifa za wanaoelewa dhana nzima ya ujasiriamali.

Sio nia ya makala hii kulaumu bali ni kujaribu kusaidia kuonesha njia wapi tunakwama na nini tufanye ili tuweze kuendelea. Suala hapa sio kusubiri kupewa na kuletewa maendeleo ila ni kuhangaika na kuchakarika kwa kila hali ili kupata hayo maendeleo. Jambo ambalo ni wajibu wa kila mmoja katika nchi hii. Bila ya sisi wenyewe kuonesha tunataka nini sio rahisi mtu kutoka nje aje kutupa sisi maendeleo na kama atakuja basi anakuja kwa faida zake binafsi zaidi kuliko mandeleo yetu.

Changamoto tulizonazo ni nyingi mojawapo ikiwa ni kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya 2025 ambayo inataka Tanzania kufikia mwaka huo iwe ni nchi yenye hali bora ya maisha, iendelee kuwa ni nchi yenye amani, usalama, maelewano, na umoja, utawala bora, jamii iliyo na wasomi na elimu bora pamoja na kuwa na uchumi imara, uliojengeka na wenye kuweza kushindana na nchi nyingine duniani.

Suala la utandawazi tunaweza tu kukabiliana nalo kwa ukamilifu kama viongozi walioko madarakani wataielewa na kuitumia kwa ukamilifu dhana ya ujasiriamali. Ni muhimu tuweze kushindana katika sekta mbalimbali za maisha kiuchumi na kiutamaduni. Bila ya kusahau kuwa kila sekta hizo zina nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara na maisha bora ndani ya nchi hii.

Lakini yote hayo hayawezi kufikiwa kama viongozi tulionao hawatakuwa tayari kufanya mawazo, fikra na mielekeo yao iwe na dhana ya ujasiriamali kwa faida ya wote. Tunaelewa kuwa ni silka ya binaadamu na wako wachache miongoni mwao wanaopenda kuona wenzao wanaendelea na kufaidika kama ambavyo anafaidika yeye, sasa watu kama hao hatutaki wawe ndio viongozi wetu.

Wote walioko katika madaraka tunataka wawe na dhana halisi ya ujasiriamali ndani ya utendaji wao wa kila siku kwa faida ya wote anaowaongoza na kama tutapata viongozi wa aina hiyo nchi hii katika kipindi kifupi tu tunaweza kuwa mbali sana kwani rasilimali tulizonazo ni nyingi kama zitatumiwa ipasavyo uwezekano wa kuwa na maendeleo upo kwa haraka tu.

Migogoro tunayokabiliana nayo kama mikopo kwa wanafunzi, migogoro katika vyuo na sehemu za kazi, matatizo ya umeme, ukosefu wa hali bora ya elimu tokea shule za msingi hadi sekondari, hali mbovu na mbaya katika sekta ya afya na miundo mbinu kwa kuitaja michache inaweza kuepukwa kama walioko madarakani wataamua kukaa chini na kuielewa dhana nzima ya ujasiriamali na kuondokana na mawazo ya kwamba dhana hii iko katika biashara tu.

Kwa hali ilivyo sasa wengi wapo kujiridhisha wao binafsi, maneno mengi zaidi kuliko vitendo na hili liko katika sehemu nyingi. Ukiangalia kwa mfano mfumo wa elimu ya juu wanafunzi wanapewa nadharia zaidi kuliko vitendo, wanapomaliza na kuingia katika utendaji halisi matokeo yake ni kutokuwa na uwezo wa kiutendaji, lakini kama wangepata elimu ya vitendo tokea vyuoni bila shaka utendaji wao utakuwa ni wa hali ya juu na ni rahisi kwao kukabiliana matatizo mbalimbali ndani ya sekta husika.

Kinashindikana nini kubadilisha hali hii, leo Chuo Kikuu wanafunzi wamejazwa kama machungwa ndani ya gunia, wakati viongozi wamekalia samani za mamilioni, magari ya mabilioni semina na mikutano isiyokwisha inayogharimu lukuki ya fedha. Linapokuja suala la kuboresha mazingira na hali ya kusomea wanasema hakuna fedha za kuboresha mazingira ya elimu, hii yote ni kwamba mawazo yao hayana ile dhana ya ujasiriamali ya kutaka kujiletea maendeleo kwa haraka. Hatuna budi kubadilika.

Kama mfanyabishara anatumia muda mwingi kuwa ofisini ili kupanga mipango na njia sahihi za kuhakikisha anapata faida, inashindikana vipi kiongozi wa taasisi au shirika kutumia muda mwingi kuwa ofisini akipanga na kufikiria njia bora za kuleta maendeleo? Kwanini inapofika au hata kabla ya muda wa kazi awe ameshatoka ofisini? Kwanini siku za mapumziko asiweko ofisini kama mfanyabiashara? Tubadilike tulio na madaraka.

Nenda katika hospitali mijini na vijijini ni matatizo matupu, sitaki kuamini kuwa hatuna uwezo na fedha, kwani hoja ya kutokuwa na fedha katika dhana nzima ya ujasiriamali sio kigezo na wala sio suala la msingi, mbinu na ujanja wa kutafuta uwezo wa kujitegemea ni kigezo cha kuwa kiongozi kama hana uwezo huo huyo hapaswi kuongoza.
Hebu viongozi watumie dhana ya ujasiriamali katika utendaji wao kama vile kuwa na mawasiliano na mtandao mpana na wadau katika sekta na fani husika ili kusaidiana katika kuondoa kero na matatizo katika sehemu zao za kazi na kuwaletea maendeleo kwa haraka wahusika na sio kujinufaisha wao binafsi kama ilivyo sasa, kwani hali iliyopo sasa ni kwanza kiongozi kuwa na mazingira mazuri ofisini na nyumbani kwake tabia ambayo siyo nzuri na haiko katika dhana ya ujasiriamali.

Kama mfanyabiashara binafsi anaweza kufanikiwa na kujitoa katika lindi la umasikini na kuwa tajiri, tunashindwa wapi kutumia mbinu hizo za mfanyabiashara katika kuleta maendeleo ndani ya sekta, jamii husika? Angalia suala la umeme jinsi linavyofanyiwa kazi hadi inafika mahali unaona kuwa ni kama usanii wa aina yake hivi ndio unaoendelea kila siku kwani huwa hatupati jibu la uhakika la matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii kubwa ya watanzania.

Inasikitisha zaidi kuona viongozi hawa unapofika muda wa saa za kwenda nyumbani au siku za mapumziko hawako maofisini kisingizio kuwa sio siku ya kazi, hii yote ni kwa sababu ile dhana ya ujasiriamali imewekwa pembeni na ameachiwa mfanyabiashara mdogo ambaye ndio anaanza biashara kuwa yeye ndie anaewajibika kuhangaika kwani ndio kwanza anaanza, lakini tunasahau kuwa hii nchi na taasisi zake hazijafika popote pa kujivunia kimaendeleo.

Ningeomba dhana nzima ya ujasiriamali isisitizwe na iingie kwenye utendaji wa kila siku kwani bila ya hivyo naamini hatutoendelea katu. Suala la kujitolea kwa viongozi halina budi kuzingatiwa kwa makini sana, kwani kama umeamua kuwa kiongozi huna budi kutumia muda wako mwingi katika kufikiria na kuwatumikia unaowaongoza na hiyo ndio hali halisi ilivyo kama unataka kweli kuwaletea maendeleo wale unaowaongoza.

Suala moja ambalo ni la msingi sana ambalo wengi wa viongozi naamini kuwa ndio tatizo miongoni mwao ni mawasiliano na kutokuwa na mtandao. Inavyoonesha mengi ya matatizo yangeweza kutatuliwa kama kungekuwa na mawasiliano na mtandao miongoni mwao. Ni mara nyingi tu ndani ya nchi hii tumeona jinsi ya viongozi wanavyosigana na kupishana mawazo na maamuzi juu ya mambo mbalimbali miongoni mwao. Hii inaonyesha dhahiri kuwa ile dhana ya ujasiriamali kuwa haijawaingia ndani ya utendaji wao wa kila siku.

Kwani miongoni mwa matokeo yanayotarajiwa yanapishana badala ya kukubaliana inashangaza kidogo lakini huo ndio ukweli na ndio hali tuliyonayo ndani ya taasisi zetu mbalimbali hapa nchini na yote ni kutokana na dhana ya ujasiriamali kuwa mbali ndani ya utendaji wa kila siku wa viongozi tulionao. Haiwezekani na haiingii akilini pale viongozi wa taasisi au sekta moja kupishana mawazo na kauli juu ya jambo ambalo linatarajiwa wawe na msimamo mmoja, imeshatokea na bado hayo yanaendelea kutokea!

Hiyo yote inaonesha kuwa bado viongozi hawajaona umuhimu wa kutumia kipengele cha mawasiliano pamoja na kuwa na mtandao mpana katika taasisi au sekta zao ili kutatua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii au kundi husika. Tofauti na mfanyabiashara kwani anatumia kila nafasi ili kuhakikisha kuwa anakuza biashara yake na kuongeza wateja kwa kutumia mawasiliano jambo ambalo linawezekana katika uongozi pia.

Kama kiongozi lazima uwe tayari kukabiliana na changamoto, huna budi kuwasiliana na unaowaongoza na kujua matatizo yao na sio vibaya kushauriana na wahusika ili kujaribu kutafuta na kufikia ufumbuzi wa matatizo badala ya kukaa ofisini ukipitia makaratasi pekee. Mara zote matatizo yanakuwa rahisi kama wadau wanashirikishwa katika kuyatolea ufumbuzi kuliko maamuzi ya upande mmoja na yote ni katika mtiririko ule ule wa kuwa na mawasiliano na pande husika na ndipo dhana nzima ya ujasiriamali inapokuwa imefanyakazi inayotakiwa.

Ukiangalia taasisi mbalimbali ambazo zimepata maendelo makubwa ni kutokana na kushirikisha kuwa na mawasiliano na mtandao mpana na wadau wake katika sekta husika, viongozi wetu wanashindwa wapi nao kuwa na hali hiyo? Tuache kujiona wakubwa na watukufu tuwe karibu sana na wadau wetu, kama ni matatizo na neema ni lazima kuwa nao karibu na ndio njia pekee ya kuweza kufanikiwa, kinyume cha hapo ni migogoro na kutoelewana na matokeo ya hayo ni kutokuwa na maendeleo ndani ya sekta husika.

No comments:

At class - MUM

At class - MUM
Mazoezi ya uhariri wa picha kwa kutumia kompyuta Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro - MUM

Mjadala studio

Mjadala studio
Wanafunzi wa shahada ya kwanza mawasiliano kwa umma mazoezini studio za Muslim University of Morogoro