Search

Sunday, January 14, 2007

Nafasi ya vyombo vya habari na utendaji wake
Nitagusia kwa uchache juu ya uhuru wa kueleza na kupata habari ikiwemo kile kinacholetwa kwa jamii toka katika vyombo vya habari kupitia waandishi, watunzi na wapigapicha na zaidi nitaangalia jukumu lililopo kwa wenye fani hizo pamoja na vyombo vyao katika kuhakikisha kuwa utamaduni, utu, silka na maadili yanazingatiwa bila ya kukiuka suala la msingi la haki za binaadamu.

Hapa Tanzania hadi mwishoni mwa miaka ya themanini kulikuwa na magazeti na vyombo vichache vya habari na vyote vilikuwa vinamilikiwa na Taasisi za Serikali, hivyo habari zake zaidi ziligusia siasa na maendeleo ya nchi zaidi kuliko habari nyingine za burudani na matukio mengine ye kawaida na hata hizo za burudani zilizotolewa zilikuwa zinazingatia maadili na heshima ya jamii yetu.


Magazeti pamoja na vipindi vya redio ambavyo ndio vilichukua nafasi kubwa katika kutoa na kueneza taarifa mbalimbali kwa jamii zililenga kwa kila mtu. Hapa nikimaanisha kuwa hakukuwa na tatizo kwa gazeti hilo kulikuta ukumbini ndani ya nyumba na mtoto akasoma bila ya kuhofia wakubwa au wale waliokaribu nae kumfikiria mambo mengine sawa na vipindi vya redio vilisikilizwa na jamii au familia nzima kwa wakati mmoja.

Tofauti na hali halisi ilivyo sasa baada ya nchi kujiingiza katika mageuzi ya kiuchumi na katika kupanua demokrasia ndani ya jamii yetu. Hali iliyoko sasa hivi ninaweza kusema kuwa kila mmoja anafanya atakavyo juu ya kwamba kuna sheria na kanuni mbalimbali pamoja na wasimamizi wa sheria hizo lakini unashangaa kuona kuwa kumekuwepo na urahisi kwa vyombo hivyo na kama vile hizo sheria hazifanyi kazi au hazipo kabisa.

Kifungu cha 18 cha katiba kinazungumzia juu ya haki ya kila mwananchi “kuwa na haki ya kupewa taarifa kila wakati juu ya matukio tofauti ndani ya nchi na kwengineko ambazo ni muhimu kwa maisha na shughuli za watu pamoja na kuhusiana na mambo mengine muhimu katika jamii” hii ni haki ya msingi kabisa katika jamii yenye demokrasia kama yetu hivyo ni muhimu katika utekelezaji wake.

Lakini huwa napata taabu pale haki hii inapotumika kinyume na hasa katika mazingira tuliyonayo hivi sasa ndani ya jamii yetu hii. Naamini aidha kwa kutofahamu au kwa makusudi kabisa wako wanaotumia haki hiyo kwa kujali maslahi yao na kusahau kuwa wengine wanaathirika kutokana na hali hiyo.

Kuna mengi ambayo yanafanyika kupitia vyombo vya habari hapa nchini. Utaona magazeti hasa yale yanayosemwa kuwa ni “magazeti pendwa” yakiwa na habari na picha ambazo kwa mujibu wa waliobobea katika fani wanasema ni vigumu kuona hali hiyo katika vyombo vya habari nchi zilizoendelea na jamii iliyostaarabika, sasa huwa nashangaa kwa nini hapa kwetu hiyo hali inaachwa ikiendelea hali wataalamu, sheria pamoja na vyombo vya kusimamia hizo sheria vipo zinaangaluia tu au kwa vile hatujaendelea?

Kutoa picha zenye kuonyesha hali halisi ya mazingira ambayo mtu amekufa, wengine wamejeruhiwa, damu zimetapakaa kila mahali, picha za uchi na nyingine nusu uchi, kuandika habari za matusi waziwazi, kuandika vichwa vya habari ambavyo ni tofauti na habari zilizoko ndani haya ni machache tu kwa upande wa magazeti.

Ukija kwenye televisheni na redio huko nako kuna yake, jinsi nyimbo zinazooneshwa pamoja na uchezaji wake picha zake hazifurahishi kila mtu na kwa maadili ya jamii yetu ni kwamba hazifai. Redio nyimbo zinazoimbwa unashangaa kama kuna wahariri, matusi ya moja kwa moja ni ya kawaida ndani ya nyimbo hizo, nyingine zikisifia bangi na vileo vingine ambavyo kisheria haviruhusiwi, ni uhuru wa kujieleza?!!

Kwa ujumla huu unaoitwa uhuru wa kujieleza “Freedom of Expression” kwa hapa nchini, mimi kwa mtazamo wangu uhuru huu unatumiwa vibaya na hatuna budi kuanza kupeana taarifa na kuelimishana kuwa uhuru huu unakuwa kero na wenye athari kwa wengine hali ambayo kisheria ni makosa. Uhuru anaokuwa nao mmojawapo usizidi mipaka na kuathiri wengine kwani unakuwa sio uhuru tena bali ni uvunjaji wa sheria.

Kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa upande wake, kama ni mpigapicha kwanini ukapige picha inayoonesha kwa ukaribu kabisa maiti, kwani hiyo maiti haina wenyewe, kwani hao wahusika hawaumii wanapoiona hiyo picha katika mazingira hayo, mbali ya wao unafikiria nini kwa wengine ambao picha za aina hiyo zinawaathiri kisaikolojia kwa ujumla. Tunapaswa kuzingatia maadili na miiko ya kazi zetu.

Inajulikana wazi kuwa kama ni mwandishi kuna mipaka na maadili ya kazi ambayo inapaswa kuzingatiwa, kuenda kinyume na mipaka na maadili hayo ni kutofuata utaalamu unavyotaka na hivyo atendaye hayo hapaswi kuwa ndani ya hiyo taaluma au wafanyayo hayo sio wataalamu halisi ndani ya hiyo taaluma, je tuseme walioko katika kazi sio wataalamu? Na kama sio wataalamu walipataje vibali na ruhusa za kufanya kazi ambayo hawana taaluma nayo?

Haya ni baadhi ya maswali ambayo huwa najiuliza mara kwa mara, hivi kweli tuna viongozi katika taaluma? Tanzania kwa bahati nzuri tuna vyama vya waandishi wa habari, tuna baraza la habari je haya hawayaoni? Au ni kuyafumbia macho tu kwa vile hakuna aliyelalamika, tunasubiri hadi watu walalamike ndio tuone majukumu yetu?

Inaeleweka wazi kwa walio kwenye taaluma ya uandishi kuwa vyombo vya habari vina wajibu ambao haukuandikwa popote pale ila kutokana na fani yenyewe ilivyo huwa wanapaswa kulinda maslahi ya jamii, je hii hali iliyoko sasa hivi kweli maslahi ya jamii yanalindwa kutokana na kinachoandikwa, kuonyeshwa na kurushwa hewani na vyombo hivyo?

Vyombo vya habari vinapaswa kuendeleza na kulinda jamii, leo kwa jinsi ya vitu vinav yoandikwa, kurushwa hewani toka kwenye redio na televisheni siamini kwa mtazamo wangu mdogo nilionao kuwa vinasaidia jamii yetu zaidi ni kuipotosha. Hebu na tuangalie nchi za wenzetu tusijali maslahi yetu tu kwa vile tunafanya biashara, hii nchi ni yetu sote wanaoathirika na tunachowapa toka kwenye vyombo hivi ni watu wetu hivyo kama ni hasara ni kwa taifa zima letu wenyewe wakiwemo ndugu na jamaa zetu na sio watu wa nje.

Ni wajibu ambao upo kutokana na misingi ya kiutu na kibinaadamu hivyo tunaopaswa kuuzingatia. Leo unaporushwa hewani video inayoonesha vijana wakisifia bangi au video yenye kuonyesha vijana wakicheza nusu uchi au nyimbo zinazozungumzia mambo ya chumbani unategemea nini katika jamii na kama sio wale waliochini ya uwezo wa kufikiri mbali na kujua athari zake ambao ndio wengi katika nchii hii wanapoiga na kuamini ni mambo ya kawaida kwani hadi kufikia kuoneshwa kwenye vyombo vya habari ni kwamba yamekubalika, halafu tunalalamikia wazazi kuwa hawawajibiki vya kutosha katika malezi ya vijana.

Inaeleweka wazi jinsi vyombo vya habari vinavyoweza kubadilisha jamii, leo hii ni vitu vya kawaida kwa mtoto ndani ya nyumba kumuambia mzazi wake kuwa “wewe hujui hiyo, hujaangalia au kusikia kwenye redio kuhusu jambo hili” kwa jinsi ya uwezo mkubwa wa kushawishi ulionao vyombo hivi na kwa vile maisha yamebadilika vyombo vya habari vinakuwa ni mzazi mwengine kwa vijana kwani muda wanaotumia kuwa navyo ni mwingi zaidi kuliko anaokuwa nao mzazi kutokana na shughuli na mihangaiko ya maisha ilivyo.

Suala la kuheshimu haki za wengine ni jambo ambalo kwa ujumla vyombo vya habari vya nchi hii vingi vimelisahau kupitia makala, vipindi na picha mbalimbali inazozitumia. Suala la athari kwa jamii au mtu mmoja mmoja halijapewa nafasi yake, umefika wakati wa vyombo vya habari kuliona na kulizingatia hilo katika jamii yetu hasa katika kipindi hiki cha utandawazi ambapo wanaoona mbali wanaweza kutumia nafasi hiyo kuja kushawishi waathirika wafungue kesi na kuweza kujipatia fidia.

Mbali ya kuwa tuna sheria nyingi tu zinazoratibu shughuli mbali mbali za waandishi pamoja na kinachoandikwa naamini bado kuna kazi ya ziada inahitajika kufanyika ili kuondoa hali hii iliyopo sasa. Dhana ya kuwajibika kwa jamii toka kwa vyombo vya habari inatakiwa kupewa kipaumbele na nafasi yake, serikali haina budi kuchukua hatua ili kulinda uhuru wa wananchi wake zikiwemo hatua za kupiga marufuku utoaji wa picha, maneno na kila chenye kuleta hisia mbaya kwa wahusika pale inapowezekana

Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika jamii, mojawapo ni kujenga uaminifu kwa jamii, vinatakiwa vitoe na kuandika ukweli, wenye uhakika, usio na athari kwa upande wowote, wenye kuzingatia mwelekeo na usiopitwa na wakati. Vinatakiwa viwe huru lakini vyenye kuzingatia na kujirekebisha pale wanapofanya makosa. Umakini katika kufuata mipaka na sheria za kitaaluma na pia vikubali kuwa katika mazingira mengine serikali inaweza kuingilia kati ili kulinda maslahi ya jamii.

Vyombo vya habari vimekuwa vikipokea na kurusha hewani picha pamoja na muziki ambao hauna maadili kabisa katika jamii yetu. Sasa hivi hakuna tofauti yoyote kati ya vyombo binafsi na vile vya serikali kutokana na kinacholetwa kwa jamii kama ipo basi ni ndogo sana. Maneno yaliyoko katika muziki pamoja na picha zake hazina heshima, lazima tukubali sio utamaduni wetu tunaiga bila ya kujiuliza ni kwa faida ya nani na zinatusaidiaje katika malezi na makuzi ya vijana katika jamii yetu.

Kuna watakaosema kuwa kwani si nyimbo tu ina madhara gani na makuzi ya vijana. Hapa hatuna budi kuangalia nyimbo zinawakilisha nini katika jamii, ni utamaduni na utamaduni ni mfumo wa maisha ya kila siku ya jamii husika. Kinachoimbwa au kuonyeshwa ndani ya vipindi na muziki ni utamaduni wetu kweli? Ni kweli hayo ndio maisha yetu na je tunakubaliana nayo? Ni kweli kuwa hayo ndio maisha yetu ya kila siku?.

Sikatai hoja ya kuwa walioko ndani ya fani ya uandishi ni vijana ambao ndio wengi na hivyo moja kwa moja kile kinachozalishwa kitakuwa na sura hiyo hiyo ya walioko ndani ya fani. Lakini tuende mbele na kurudi nyuma, je tunajenga au tunabomoa Taifa letu? Wale walio wadogo zaidi wanajifunza nini na wanapata faida gani kwa maendeleo yao ya baadae kwani wanapoangalia, kutazama na kujisomea upuuzi wanajifunza nini, lazima tuzingatie kwa uangalifu mkubwa wanachopata kwani ndicho watakachokuwa wanakitumia katika maisha yao ya kila siku hapo baadae.

Inataarifiwa kuwa Afrika hivi sasa asilimia 33 ya watu wake ni vijana (Ashford, 2006). Vijana hawa nakabiliwa na changamoto kubwa katika elimu, familia, ajira na masuala ya afya. Kuna tofauti kubwa kati yao na wale wa miaka ishirini iliyopita. Na kinachochangia katika kuleta changamoto hizo mbali ya suala la utandawazi, ukuaji wa teknolojia na nguvu za kiuchumi, vyombo vya habari navyo vinachangia kwa sehemu kubwa changamoto hii.

Juhudi zinazofanywa na Jumuia ya Waandishi wa Habari Kusini mwa Afrika (MISA) katika kipengele cha kujaribu kuondoa umasikini kupitia vyombo vya habari zinapaswa kuzingatiwa kwa undani. Umefika wakati wa kuwawezesha wananchi na vijana kwa ujumla kupitia muziki, taarifa na vipindi mbalimbali ili kubadilisha na kupanua uwezo wao wa kufikiri badala ya kutumia vyombo hivi kuwapa mawazo ya mapenzi, starehe na ngono tu kama ilivyo sasa.

Waandishi, watengenezaji na wataarishaji wa vipindi vya televisheni na redio hawana budi kubadilisha au niseme kuzingatia zaidi kutoa changamoto na mawazo ya kujikwamua na umasikini katika elimu, afya, mazingira na masuala yote muhimu katika ustawi wa jamii. Suala la kuangalia asilimia 95 ya vipindi, habari zihusuzo mapenzi na starehe linapaswa kupigwa vita kwa kila hali na ni kupitia vyombo vya habari tu suala hili linaweza kupata ufumbuzi.

Hili liliwezekana katika miaka ya sitini kwanini lisiwezekane sasa? Na kama haliwezekani je wahusika ikiwemo serikali wana mkakati gani katika hili? Tunapaswa kujiuliza tunatoa leseni na uhuru wa watu kujieleza lakini una manufaa kwa jamii au ndio uhuru bila ya mipaka. Walioko katika vyombo hivyo wanapaswa kujiuliza wajibu wao kwa jamii ni upi, kuwaletea habari za mapenzi na starehe tu au kujaribu kuendeleza jamii husika kwa kuwaelimisha na kuleta chachu ya maendeleo katika akili zao kutokana na wanachoangalia, kusoma na kusikiliza?

Matatizo ya madawa ya kulevya, afya ikiwemo malaria na Ukimwi ni mojawapo ya changamoto zinazokabili vijana barani Afrika na Tanzania kwa ujumla. Wakati umefika wa kuburudishana kwa kupanua mawazo ya jinsi ya kupambana na matatizo yaliyoko badala ya kufikiria na kuendelea kufanya starehe tu ambazo katika maisha na mazingira yetu hazina mwisho mwema.

Mfano tunaporuhusu kuwa na fulana, kofia, na mapambo mengine yenye kusifia bangi zikivaliwa na vijana wakati bangi yenyewe ni marufuku kuitumia ukweli mtu unashindwa kuelewa nini maana yake. Leo imekuwa ni kawaida tu kwa tabia hiyo na wla hakuna anayesema lolote kwa sababu ni uhuru wa kujieleza na suala la utandawazi, lakini jee nini madhara yake, kweli kijana atavaa tu nguo yenye bangi bila ya kutumia na kuona hali halisi ya hiyo bangi kweli?

Matangazo ambayo kwa ujumla wake hayaonyeshi madhara halisi kwenye matumizi ya vileo, sigara na starehe nyenginezo tunategemea nini kwa Taifa hili hapo baadae? Serikali kwa ujumla wake inapaswa kujipanga upya na kuwa na mikakati ya kuboresha sekta ya filamu, uzalishaji wa matangazo na yale yote yanayoletwa kwa jamii ili yaweze kuwa na matokeo mazuri badala ya hasara kwa Taifa.
Sina maana ya kuzima uhuru uliopo hivi sasa, ila uhuru huu uliopo uwe na manufaa kwa pande zote mbili wanaozalisha na wanaopokea kwa matumizi yao ya kila siku kuliko hii hali iliyoko sasa. Ni kweli soko la ajira limepanuka kutokana na uhuru huu bado kuna kazi kubwa iliyoko mbele ya kutengeneza mazingira yatakayokuwa na faida kama vile kuifanya na kuipa nafasi yake hii sekta ya uzalishaji wa filamu, miziki na machapisho mbalimbali katika jamii yetu kutoa ajira na kutoa hali halisi ya sura ya utamaduni wetu.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa sekta hii haijapewa nafasi kama sekta nyingine kama nchi zilizoendelea imefanya. Ni karibuni tu ndio kumekuwepo na vyuo vikuu vinavyotoa elimu ya juu kwa walioko katika fani za uandishi hapa nchini. Na vile vile kwenye fani ya sanaa wengi wameingia humo kwa lengo la kujifaidisha wao binafsi na sio kulinda maslahi ya jamii, lakini hayo yote yasitupelekee kuwa na uhuru usio na mipaka, sheria zizingatiwe ili kuwe na mustakbali mwema kwa jamii yetu sasa na hapo baadae.

No comments:

At class - MUM

At class - MUM
Mazoezi ya uhariri wa picha kwa kutumia kompyuta Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro - MUM

Mjadala studio

Mjadala studio
Wanafunzi wa shahada ya kwanza mawasiliano kwa umma mazoezini studio za Muslim University of Morogoro